Sunday 17 June 2012


Virutubisho Vinavyopatikana Katika Vyakula

Mwili wa binadamu (na viumbe vingine hai) ili uweze kukua na kunawili unahitaji vitu vinavyojulikana kama virutubisho au viinirishe. Kwa lugha ya kigeni virutubisho vinaitwa “Nutrients”. Virutubisho hivyo vinapatikana katika vyakula mbalimbali.


Vile vile tunajuwa kuwa, virutubisho vyote hugawanywa katika makundi makuu sita, ambayo ni kabohaidreti (wanga, sukari na nyuzi nyuzi), protini, mafuta, vitamini, maji na madini (minerals). Ili mwili uweze kukua na kunawili vizuri lazima upate virutubisho vyote.

Chakula (kama cha asubuhi, mchana, jioni au usiku) chenye virutubisho vyote sita hujulikana kama mlo kamili au “balanced deit” kwa lugha ya Waingereza. Kwa vile takribani vyakula vyote tunavipata kwa gharama kubwa (fedha au kazi), swala la uchaguzi wa vyakula haliepukiki.

Pia unategemea mazoea ya mlaji, radha na sura ya chakula, virutubisho na mambo kadhaa wa kadhaa. Ili kufikia uchaguzi sahihi wa vyakula, elimu ya chakula gani kina virutubisho gani ni ya msingi. Jukwaa ili linakusudia kukidhi haja hiyo kwa wasomaji wote. Katika kukidhi haja hiyo, vitataja aina ya chakula, virutubisho vya msingi na virutubisho vya ziada vinavyopatikana katika vyakula hivyo.

Nafaka:
Nafaka ni vyakula vya punje punje au chembechembe kama vile mtama, mahindi, ngano, uwele (mawele), mpunga n.k. Virutubisho vya msingi vinavyopatikana katika vyakula vya nafaka ni wanga, sukari na nyuzi nyuzi. Virutubisho vya ziada ni Protini, vitamini (kundi la B) na baadhi ya madini.

Vyakula jamii ya mizizi na matunda
:

Vyakula jamii ya mizizi (starchy roots) ni kama vile viazi (vitamu, mviringo, n.k) mihogo, n.k. Virutubisho vya msingi vinavyopatikana katika vyakula jamii ya viazi na matunda ni wanga, sukari na nyuzi nyuzi (dietary fibres). Zaidi ya virutubisho hivyo ni baadhi ya madini, vitamini C (kama chakula hicho siyo kikavu) na vitamini A (kama chakula hicho kinarangi ya njano).

Vyakula jamii ya maharage
:

Vyakula jamii ya maharage nikama vile maharage ya kawaida na yale ya soya, kunde, choroko, n.k. Virutubisho vya muhimu katika kundi la vyakula vya hapo juu ni wanga, protini na nyuzi nyuzi. Virutubisho vya ziada ni vitamini (kundi B) na madini.

Mbegu za mafuta
:

Mbegu za mafuta ni kama vile alizeti, pamba, ufuta, nazi, mawese (chikichi), kweme, maboga, tikiti maji, matango, n.k. Virutubisho vinavyopatikana kwa wingi katika mbegu za mafuta ni mafuta, protini na nyuzi nyuzi. Ziada kundi B. (B- Vitamins).

Nyama/Samaki
:

Virutubisho vya msingi katika nyama au samaki ni protini, mafuta na madini ya chuma. Virutubisho vingine ni vitamini vya kundi B na madini (zaidi ya yale ya chuma).

Ini
:

Ini linatupa virutubisho vya msingi vya protini, madini ya chuma na vitamini.
Maziwa:
Virutubisho tunavyovipata kwa wingi katika maziwa ni mafuta, protini, baadhi ya madini na vitamini.

Mayai
:

Mayai yana virutubisho vya msingi vya protini na vitamini. Zaidi ya hivyo ni mafuta na madini (siyo ya chuma).

Mafuta
:

Mafuta kama chakula yanatupa mafuta kama kirutubisho cha msingi. Zaidi ya hicho ni uwezekano wa kupata vitamini A.

Mboga za majani
:

Mboga za majani hasa zile za kijani zinavirutubisho vya msingi vya vitamini A, C na B, Zaidi ya hivyo ni protini, madini na nyuzi nyuzi.

Matunda jamii ya machungwa
:

Matunda jamii ya machungwa ni machungwa, machenza, n.k virutubisho vya msingi tunavyovipata kutoka katika matunda jamii ya machungwa ni sukari, vitamini A na C. Zaidi ya hivyo ni madini na nyuzi nyuzi.

0 comments:

Post a Comment

Subscribe to RSS Feed Follow me on Twitter!