Sunday 27 October 2013


MARA nyingi yanapojitokekza maradhi ya kipindupindu na yale ya homa ya matumbo (typhoid fever) viongozi wa kisiasa huwahamasisha wananchi kuchemsha maji ya kunywa.

Kuhusu zoezi hilo baadhi ya wananchi hujiuliza maswali, moja ya maswali hayo ni hili:

Wataalamu na wafanya kazi wa mamlaka mbali mbali za maji hutuambia kuwa, maji yanayosambazwa kwenye mabomba kwa baadhi ya miji kama vile Dar es Salaam, Tanga na Morogoro yanatiwa dawa ya kuua vijidudu vinavyoambukiza maradhi, kwanini tena tunaambiwa tuyachemshe maji ya aina hiyo?
Swali hili la wananchi lina mantiki hivyo basi linahitaji majibu ya kisayansi, vinginevyo wananchi wanaweza kuupuzia wito huo muhimu wa viongozi wetu.

Tatizo linakuwa kubwa zaidi juu ya hoja ya hapo juu kwa vile, viongozi wengi wa kisiasa huwa hawatoi maelezo ya kina ni kwa sababu gani maji yaliyotiwa dawa yanahitaji kuchemshwa. Makala yetu ya wiki hii inalenga katika kujibu swali la wananchi tuliloliona hapo juu.

Maji ya bomba yanayosambazwa katika miji yetu hapa Tanzania yanatoka katika vyanzo mbali mbali kama vile mito, maziwa, mabwawa, chemchem, visima n.k. Mamlaka za maji safi na maji taka katika miji yetu mbali mbali zinajitahidi kuyasafisha na kuyatia dawa maji hayo.

Wananchi waliopata bahati ya kutembelea mitambo ya kusafisha maji ya kunywa wanajua kazi ngumu na gharama kubwa inayoipata serikali yetu (au serikali nyingine) katika swala zima la kusafisha na kusambaza maji ya kunywa.

Hata hivyo, mara kadhaa maji yanayosambazwa kwenye mabomba huwa si safi wala si salama. Hii haina maana kuwa maji hayo yanasambazwa bila ya kusafisha au kutiwa dawa. Maji yanasafishwa na pia yanatiwa dawa, lakini kuna kasoro za kiufundi na sababu za kiuchumi zinazofanya maji yaliyosafishwa na kutiwa dawa yamfikie mteja (mtumiaji) hali ya kuwa si safi wala si salama.

Kwa maneno mengine, mara nyingi katika baadhi ya miji yetu maji huwa safi na salama pale katika mitambo. Lakini yanachafuka wakati wa kuyasafirisha kwa watumiaji. Kasoro hiyo inachangiwa na sababu nyingi, baadhi yake ni hizi.

Uchakavu wa Mabomba 

Mabomba mengi yanayosambaza maji katika miji yetu ni ya zamani, mengine yaliwekwa enzi ya Wakoloni. Mabomba mabovu huingiza uchafu katika maji hasa kama nguvu (pressure) ya maji katika mabomba ni ndogo. Ufumbuzi wa kasoro hii ni kuweka mabomba mapya. Lakini kikwazo ni uwezo mdogo wa kifedha wa serikali! Kwa hoja hii lazima wananchi wachemshe maji hata kama maji hayo yalitiwa dawa katika mitambo (au matanki ya kuhifadhia maji), la sivyo wananchi tutakwisha kwa magonjwa kama vile kipindupindu na homa ya matumbo.

Kupasuka kwa Mabomba 

Mara nyingi mabomba ya wananchi (mitaani) hupasuka kwa sababu mbali mbali, mojawapo ni kupasuliwa na magari au watoto. Bomba linapopasuka huwa ni sababu ya maji safi na salama kuchanganyika na uchafu, hasa kama nguvu ya maji katika bomba ni ndogo. Hali inakuwa mbaya zaidi kwa maeneo ambayo uchafu hutandaa katika maeneo yanayopita bomba.
Jambo la kufanya ni kuwa wananchi tuyaweke mazingira yetu katika hali ya usafi na pia mabomba lazima yachimbiwe kina cha kutosha.

Vijidudu Vilivyojeruhiwa 

Kwa kawaida wataalamu wa maji safi (maji ya kunywa) huwa wanachunguza ubora wa maji. Katika kazi hiyo huwa wanapima pamoja na vitu vingine, vijidudu vilivyo hai katika maji. Kama hawakuviona vijidudu hivyo, hujua kwamba maji yamesafishwa vizuri. Hivyo huyaruhusu kusambazwa kwa wananchi.
Hata hivyo, maji hayo yanaweza kuwa na vijidudu kabla ya kumfikia mnywaji na hapa sasa sababu yake siyo uchafu wala uchakavu wa mabomba. Sababu yake hapa ni vijidudu vilivyojeruhiwa, kwa Kiingereza vinaitwa injured/stressed microorganisms.

Vijidudu vilivyojeruhiwa (kuzimia) huwa na uwezo wa kufufuka vinapopata mazingira mazuri kama ya kuwepo dawa kiasi kidogo katika maji. Hoja hii ni ngumu kidogo kwa watu ambao si wataalamu wa sayansi ya vijidudu (microbiology). Hata hivyo, jambo la kuzingatia kwa watumiaji wa maji ni kuwa, mara nyingi wataalamu wa maji hawavichunguzi hivi vijidudu v ilivyojeruhiwa. Kwa hiyo vikipata uhai huwa ni hatari kwa afya ya watumiaji wa maji.

Kwa kuzingatia falsafa hii ya vijidudu vilivyojeruhiwa ninawaomba wataalamu wa maji kuvichunguza vijidudu hivi wakati wanapopima ubora wa maji. Kwa hakika ninajua ugumu na gharama ya kuvichunguza vijidudu hivyo, lakini afya ni bora kuliko mali, ndiyo maana katika baadhi ya nchi vijidudu hivyo huwa ni lazima kuvichunguza unapopima ubora wa maji.

0 comments:

Post a Comment

Subscribe to RSS Feed Follow me on Twitter!